Wanawake wengi kwa sasa wanalalamika namna wanaume walivyo kwenye
mahusiano, wanasema wanaume wamepoteza moyo wa dhati wa kuwepo wenye
mahusiano yaani “commitment”, wanaonekana kama hawana mapenzi tena, wao
kila siku ni kuuliza tu tendo la ndoa, na kama halipati basi anaweza
kuondoka muda wowote kuelekea huko anakolipata tendo hilo.
Hali hii inasumbua mahusiano mengi ya uchumba na wengine wamelazimika kuvunja uchumba, wakiwa karibia kuingia kwenye ndoa.
Wanawake
hawa wanalalamika wakisema wako wapi wale wanaume wenye kiu ya ndoa?
Wako wapi wale wanaume wenye kuongelea kutaka kuoa na kuanza familia na
kuwapenda watoto wao? Wako wapi wale wanaume wenye kiu ya mafanikio na
kudumisha maisha pamoja na wake zao, mbona kama wamemalizika na
waliobaki wana kiu za kula bata tu “kufanya starehe” na kufanya mapenzi
pasipo kumaanisha.
Yamkini na wewe unayesoma makala hii
unajiuliza maswali haya pia. Wanawake wengine wamekuwa wakieleza kuwa
wanaume waliobaki siku hizi ni wavivu, hawana hamasa ya maendeleo,
atakuwa na wewe kama ana uhakika wa tendo la ndoa tu.
Leo nimekuja
kuzungumza na wasichana na wanawake ambao nao wanamawazo na maswali
kama haya, ni kweli vilio na malalamiko yenu ni ya kweli na tunasikitika
pamoja kwenye hili lakini pia tafiti zinasema iko sababu ya hali hii.
Ni
vyema mkafahamu kuwa kwa kiasi kikubwa mifumo au mbinu za mchezo wa
mahusiano zimebadilika sana, nadharia za zamani nazo zinaonekana
kubadilika na hii imewafanya wanaume wengi kubadili aina ya maisha yao.
Fuatilia
sababu zifuatazo ili kulielewa hili sawia. Kumbuka kuwa sababu hizi
zimetokana na majibu ya wanaume wengi kwenye tafiti;
Mgawanyo wa majukumu baina ya wanaume na wanawake umeingia doa.
Wanaume
wa kawaida hupenda kufanya kazi ili kujitafutia kipato chao na familia,
na wakitoka kazini au kwenye majukumu yao ya kila siku wanataka
kupumzika na kufanya kile wanachojisikia kufanya iwe ni kulala,
kuangalia televisheni, kusikiliza redio n.k na sio kukimbizana na
vijishuhuli vya nyumbani kama vile kusaidia kupika, kusafisha vitu,
kukaa na watoto na kazi nyingine ambazo wao wanaona sio zao.
Ndani
yao wanakiu ya kuona wapenzi wao wanawakaribisha kwa upendo,
kuwaandalia maji, kuwasaidia kuweka mazingira ya wao kupumzisha akili na
mwili baada ya kula chakula, wanakiu ya kuona tabasamu, sauti nzuri, na
ikiwezekana kupata penzi. Kwao hali hii kuwapa nguvu tayari kuwaandaa
na siku nyingine ya kesho.
Tatizo linakuja pale mwanaume huyu
anajikuta ameoa mwanamke mfanyakazi au mwenye majukumu mengi yamkini
kumzidi hata mume, akikaa, akilala anawaza kazi, anawaza biashara
anawaza miradi na vingine vingi, akirudi nyumbani mwanamke huyu anakuja
amechoka na hajiwezi kimwili na kiakili kama vile vile alivyo mume wake,
mke na mume wote wamechoka sana, mke na mume wote wana msongo wa mawazo
na wanahitaji kupepewa maana hawajiwezi kwa kuchoka.
Mwanamke
amechoka hana hamasa ya kufanya kazi ndogondogo za nyumbani au hata
kuwashuhulikia watoto. Ulimwengu wa kazi na majukumu umeshamfanya
mwanamke kuwa na misuli ya kukimbizana na maisha kama mwanaume.
Hali
hii inawafanya wote wawili wanarudi nyumbani wamechoka kabisa na kila
mmoja anauhitaji wa msaada wamwenzake wakati hakuna aliyetayari wala
aliyena nguvu ya kumsaidia mwenzake. Katika hali kama hizi vijihasira na
vihisia hasi huamka kwa urahisi sana na magonvi huweza kupenye
hapohapo. Ule uwiano wa masaidiano umeshapotea na kilichoota ni hatari
sana kwa mahusiano ya wawili hawa.
Wachunguzi wanasema ndio maana
zipo jamii na imani fulani ambazo mke huachwa nyumbani akimsubiri mume
wake na mume kazi yake ni kuhakikisha anafanya kila jitihada kuilisha na
kuitunza familia, sio kwamba hawataki mke afanye majukumu ya baba la
hasha, wanamuandaa kuweza kumhudumia mumewe vilivyo. Najua hoja za wengi
pia zina mashiko kwamba wanawake wengine wangependa kukaa ka
kuwasubiria waume zao ili wawaenzi lakini wanaume wengine wameshindwa
kubeba majukumu yao kama wanaume na viongozi wa familia na hiyo
imewalazimu wanawake kusimama na kufunga mkanda. Pamoja na hayo hali ya
masumbufu haijapungua.
Wanaume hawapendelei kulipia kitu wanachoweza kukipata bure.
Ni
dhahiri kabisa kwamba wanawake wengi sikuhizi hata wale wenye umri wa
kuolewa wamejikita zaidi kwenye maisha ya starehe, wao ni kula, kunywa,
kusafiri, kuvinjari usiku hadi kukuche wanakula maisha “wanakula bata”.
Ngono imekuwa rahisi sana kwa wasichana wa umri mdogo na hata wanawake
waumri wa kuolewa na pia wale walioko kwenye ndoa.
Unakuta
mwanamke anakiu ya kuolewa na anasema wazi kuwa anatamani kuwa na mume
lakini maisha nayoishi hayaendani kabisa na mke wa mtu, anashindwa
kufahamu kuwa waoaji wengine ndio hao hao anashinda nao baa na kwenye
majumba ya starehe, anashindwa kujua kuwa watu wanamwona na wanapata
picha dhahiri ya namna na tabia aliyonayo. Vijana wanaona kama ngono
inaurahisi wakuipata hivyo yanini akajitutumue kuanza michakato ya
kulipa mahari? Kama unaweza kumwambia mwanamke aje kwako na akalala wiki
pasipo shida, kunahaja gani ya kubeba kajukumu mengine ya zaidi?
Waingereza wanasema “if you can affor a sousage why keeping a pig” (Kama unauhakika wa kupata nyama ya nguruwe kwanini uhangaike kumfuga?).
Usitegemee
kuolewa na mtu mzuri, anayemaanisha na mwenye mapenzi wakati wewe
haumaanishi chochote na penzi lako unagawa kwa yeyote huko nje. Kwa
taarifa yako hata mwanaume aliyeko kihasarahasara anakiu ya kuwa na mke
anayejiheshimu. Ningumu sana rafiki zako wa kiume wanakaa na wewe hadi
kunakucha wanakurudisha kwenu au kwako halafu unadhani yuko kati yao
atakaye kuja kusema anataka kukuoa, never!! Kila anayekuona anajua fika
wewe sio mke ni mwanamke wa usiku, utakachokipata sanasana ni kufanya
nao ngono, wakuache hapo waende zao kuoa wanawake wanaojielewa.
Majukumu ya baba kama kichwa cha nyumba yamebadilika
Kwa
asili wanaume wameumbwa na kiu ya kutaka kuongoza, kutaka kuwa
wasimamizi au wakurugenzi wakila kitu kwenye maisha yao, kwenye vipaji
vyao, kwenye kazi zao, kwenye mahusiano yao na hata kwenye familia zao.
Pamoja na kiu hii, kwa miaka ya karibuni hali imebadilika sana,
maendeleo ya kijamii na kiteknolojia yamepunguza sana au kuondoa kabisa
ule ukuu alokuwa nao baba kwenye familia yake.
Leo kwenye jamii
nyingi hususani za magharibi baba hawezi tena kumuadabisha mtoto wake
maana anaweza kumshtaki kwenye vyombo vya sharia au hata kumpeleka
mahakamani. Leo katika jamii nyingi duniani, kwenye nchi zilizoendelea
na hata hizi zetu zinazojikongoja, baba akisema atumie mamkala yake kama
baba haiitwi tena mamlaka inaitwa unyanyasaji, na inaweza kumtokea mtu
puani. Kila mke anataka usawa, ukifanya hivi mke atafanya vile, ukitaka
hiki nayeye atataka kile, ndoa nyingi zimeshakuwa kama chama tawala na
chama cha upinzani, wanandoa wengi wameanza kuishi kama taasisi sio kama
wapenzi. Inasemekana kwamba kama ile kiu ya baba au mwanaume kuhangaika
na kuwekeza jasho na akili yake kwenye familia yake ili aiongoze, awe
kichwa imeoza au haileti faida basi hakuna anayeona umuhimu wa jitihada
hizo tena. Imekuwa kama mfanya biashara anaona yanini kuwekeza ambako
unauhakika patakupa hasara? Maana ya hii ni kwamba, hamasa ya wanaume
wengi kuingia kwenye ndoa na hatimaye familia imeonekana kupungua na
hivyo kulitafuta hitaji lao la asili ya tendo la ndoa nje ya ndoa.
Sheria za ndoa zinawabana wanaume zaidi
Wanaume
wengi wameonyesha kuhofia sharia za ndoa kwa jinsi zinavyomgandamiza
mwanaume na kumpa chapuo mwanamke. Wanaume wengi walioliongelea hili ni
wa jamii ya nchi zilizoendelea na wachache ni wanchi zinazoendelea,
wanasema wanahofu ya kuingia katika makubaliano tena ya maandishi ya
kuishi pamoja maishani wakati makubaliano hayo yanamlemea mtu mmoja na
sio wote, husuani pale mambo yanapoonekana kuharibika na tofauti
zikaibuka baina ya wawili hawa.
Nyakati ndoa zinapovunjika na
wanandoa wakalazimika kuchukulia mambo kisheria, mwanaume anahofia
kupoteza kila anachoona ni chamuhimu kwake. Pamoja na kwamba upo ukweli
kwamba hata kama mwanaume ndiye alitafuta lakini kuna watoto nao
wanatakiwa kufaidika au kuendelezwa pamoja na kwamba ndoa imeshindikana,
lakini wengine wanasema hatakama hatuna watoto, bado mwanamke ananafasi
kubwa ya kumbana mwanaume kisheria. Pamoja na kwamba hofu hii
haionekani sana kwa wanaume wanchi kama ya kwetu ila wapo baadhi wenye
mtazamo huu. Kwa mtazamo huu sasa wengi wanaona bora waendelee kutafuta
haja ya mwili “tendo la ndoa” halafu hayo mambo ya kuishi pamoja kama
mume na mke yatajulikana huko mbele yasafari.
Hamasa ya kukua na kupevuka imepungua
Kuendesha
familia au kuwa baba bora wa familia kunahitaji sana kumaanisha na
kujitoa “commitment”, pasipo tabia hizi utabaki kuitwa baba au mume
lakini lazima kutakuwa na mapungufu mengi sana na malalamiko kwenye
familia kutoka kwa mke na hata watoto.
Kwa bahati mbaya
inaonekana tabia hizi za kumaanisha zinapungua kwa kasi sana kwa
wavulana wengi wenye umri mdogo na kuendelea hadi wanapokuja kuwa vijana
wakubwa wanaotarajiwa kuingia kwenye ndoa zao. Vijana wanaonyesha uvivu
na kukwepa majukumu wakiwa wadogo, wanachukia kazi na kuwa walegevu,
wanapenda vitu virahisi na maisha ya anasa tu, mtu anatamani aangalie
televisheni siku nzima na asifanye kazi. Familia nyingi zimepwaya kwenye
suala la malezi, mvulana hapangiwi kazi wala majukumu ya kumfanya
ajitume akiwa nyumbani.
Akitoka shule basi ni kucheza na kukaa tu
na baadae wazazi hao hao waliomfundisha aina hiyo ma maisha wanakuja
kuanza kulalamika eti huyu mtoto ameharibuka wakati wao wenyewe ndio
waliomharibu. Kwabahati mbaya tabia hizi za kivivu na kilegevu na
kukwepa majukumu huendelea hadi wanapoingia kwenye ndoa.
Mtu
anaingia kwenye ndoa hata tabia ya kuhifadhi fedha yake kwa matumizi ya
baadae auya dharura hana, akipata pesa ni starehe na safari za hapa na
pale, mtu anapata mke hajui hata namna ya kumhudumia, mtoto akija ndio
kabisa vita kila siku na mke wake maana nikama vile huyo mke wake analea
watoto wawili wakati mmoja anajiita “baba”.
Inaumiza na kusumbua
sana moyo. Kwa hali hii vijana wengi wanaogopa majukumu ya familia
wanaishia kutaka tendo la ndoa tu, na hata kijana wa aina hii anapokuwa
kwenye familia hafanyi kitu cha ziada, mke ndio jembe la nyumba, kijana
yeye anasubiri kupewa unyumba tu. Kufuatia hali hii pia, baadhi ya
wanawake wamekata tama au kuchukia kuolewa, wako tayari wafurahie maisha
na kufanya mapenzi na mwanaume wanayemtaka ila pasipo masharti ya
kudumu, akihitaji mtoto basi atampata kwa muda wake bila kujali baba
ninani ama anaishi wapi. Hali imebadilika sana. Hitimisho
Ulimwengu
umebadilika sana na kuwa ulimwengu wa watu kupenda starehe, furaha na
hamasa za muda mfupi pamoja na kiu kubwa ya kufanya mapenzi hovyo.Pamoja
na kiu hiyo bado wengi wanahofia mahusiano ya kudumu na ndoa.
Wengi
wanalia kwenye mahusiano au uchumba maana hakuna kumaanisha, ni
kuumizana asubuhi, mchana, jioni nausiku. Kijana akiwa na msichana
kwenye mahusiano na akawa na uhakika wa kupata tendo la ndoa basi
anaweza hata kujisahau kuhusu kuoa, na vijana hawa kwakukwepa majukumu
wanakimbilia kuishia kwa wasichana waliotapakaa kila sehemu ambao wao ni
kula raha tu na wako tayari kumpa penzi yeyote aliye tayari kuwapa
furaha, kinywaji, na starehe nyingine, wakati haya yanatokea, wale
wanawake wachache wenye kumaanisha, wenye kujitunza, na wenye kiu ya
kuwa na familia zao wanabaki wakisubiri nani mwanaume mwenye kumaanisha
pia atakayekuja kutamani kuwa nao, maana kiukweli vijana wa aina hii ni
wakutafuta, wamepungua sana.
Pamoja na kwamba baadhi ya sababu
zilizotajwa hapo juu ni ngumu kuzizuia lakini zipo pia ambazo zinaweza
kuzuilika kama ukiweza kufanya maamuzi yako vizuri na kwa ufasaha.
Mabadiliko
ya tabia pia ni muhimu kwenye muktadha huu. Wasichana au wanawake
mnaojitunza, msikate tamaa kabisa, pamoja na kwamba dunia imebadilika na
wengi waovu ndio wanaoonekana wajanja, jipeni moyo, hakuna aliyejitunza
akajuta, ila hao wengi mnaowaona huko wakijionyesha kama wenye furaha
sana, ndani ya mioyo yao na katika nyakati wanazokuwa pekeyao,
wanamajuto makubwa sana ndani yao.
Chanzo : http://chrismauki.co.tz/index.php/2019/03/14/darasa-la-alhamisi-na-dr-chris-mauki-sababu-tano-za-kwanini-wanaume-wanataka-tendo-la-ndoa-tu-na-sio-kuoa/
Post a Comment